Mpendwa mwandishi, umetokea kuandika hadithi kwa lugha uliyoichagua. Huenda ni lugha yako unayoishi nayo. Na sasa inakwenda kutafsiriwa katika lugha tofauti – lugha ambayo huenda inafanana kidogo sana na lugha yako. Kuanzia chimbuko chake hadi sarufi, kuanzia mtindo wa sauti hadi muundo, lugha yako inaweza kuwa kiumbe tofauti sana.
Halafu kuna msomaji wa hadithi iliyotafsiriwa. Pengine,anatoka sehemu nyingine ya dunia, bila kuweza kufikia maarifa wa alama za kitamaduni unazozichukulia kuwa za kawaida kwa msomaji wako Hata maneno na misemo yakitafsiriwa kwa umakini kiasi gani kutoka kwa lugha yako kwenda kwenye lugha hii mpya, unajiuliza iwapo maana iliyodokezwa itatafsirika pia. Si jambo la ajabu uwe na hofu.
Kama mfasiri naelewa wasiwasi wako. Nina mashaka yangu pia. Ninapotafsiri, kwa mfano, hadithi ya Kibangla kwenda Kiingereza, najaa hofu: Je nitaweza kutafsiri kila kilichoandikwa katika lugha ninayoishi nayo – na si tu ninayotumia katika kuandika au kusoma – kwenda kwenye lugha ninayotafsiria. Halafu vipi Kiingereza nitakachokitumia, ambacho ni cha kwangu kwa namna ya kipekee lakini labda si Kiingereza alichokizoea msomaji wa hadithi iliyotafsiriwa?
Kupata maneno na misemo yenye maana sawa ni sehemu ndogo tu ya matatizo. Kwa uhakika, mara nyingine lugha ninayoitafsiri haitakuwa na visawe kamili lakini maana inaweza kuwasilishwa kwa kuongeza maneno au msemo na kutumia kiasi cha muktadha panapoohitajika. Ongezeko lililojificha linasuka maelezo haya katika matini, yakidumisha mtindo bila kufanya ongezeko hilo lionekane kama tanbihichini.
Aidha wafasiri wengine huacha maneno au misemo mengine bila kutafsiri ili kumwonesha msomaji kwamba yanawakilisha mambo yalio nje ya upeo wa uzoefu na maarifa ya lugha mpya. Hata hivyo suala muhimu ni kwamba utofauti unaojengwa kati ya msomaji na dhana geni usibadilishe namna msomaji anavyopokea hadithi.
Ninapotafsiri najikita kwanza kuangalia mahusiano kati ya ya lugha ‘chanzo’ ya hadithi na lugha yake sanifu – ambayo walio wengi wanasoma na kuelewa kwa urahisi. Je hadithi inatumia lugha kwa namna tofauti? Ni lugha ya majaribio? Inajaribu kubuni mambo mapya? Inatumia rejista isiyo ya kawaida? Najaribu kuhakikisha kwamba lugha ninayoitumia katika tafsiri yangu inabaki na mahusiano yaleyale na lugha sanifu, jinsi ilivyo, ya lugha ‘lengwa’. Kwa vyovyote kubadilisha mahusiano haya kutadhoofisha sana hadithi.
Kisha, usomaji wa hadithi za asili ukoje? Msomaji anapitia matini moja kwa moja? Au analazimishwa kwa makusudi kusimama na kutafakari juu ya anachosoma? Jitihada yangu ni kufanya watu wawe na usomaji wa aina hiyohiyo kwa kiasi kinachowezekana.
Mwisho kuna suala la jinsi hadithi inavyosomwa na mfasiri kabla ya kuitafsiri katika lugha mpya. Hili ni suala tata. Mimi binafsi sina njia moja tu ya kusoma hadithi tu bali nataka kuwezesha tafsiri yangu kusomeka kwa njia zote anuwai kama hadithi chanzo inavyoweza kusomwa. Lengo si kufinya mibadala bali kuihifadhi au hata kuipangua mara nyingine.
Kwangu mimi, ni muhimu kwamba tafsiri haileti taswira kwamba hadithi ilizaliwa katika lugha iliyotafsiriwa. Lakini sibadilishi kwa makusudi matumizi ya lugha ya Kiingereza ili kumkumbusha msomaji hivyo. Ukweli ni kwamba lugha chanzo hutumia manoti tofauti ambayo mwandishi huyatumia kutunga kazi inayofanana sana na muziki fulani. Kutafsiri ni kama kutumia manoti haya lakini kwa kutumia ala tofauti inayofuata masharti ya ala hii mpya na haijaribu kuwa na sauti ileile ya ala ya awali.
Kwa kifupi, mwandishi mpendwa, hadithi yako haipo tu katika maana ya kamusi ya maneno tu – ipo katika vipengele vyote hivi vingine ambavyo vinaifanya hadithi iwe hivyo. Na wakati tafsiri yake haiwezi kufanana na ile uliyoiandika moja kwa moja, ni kwa sababu tu lugha mpya ina namna yake ya kipekee. Jinsi ilivyotafsiriwa itaipa hadithi uhai mpya ambao unaweza kuwa wa kusisimua sawa na ulivyoandika wewe. Uwe na imani na mfasiri.
Imetafsiriwa kwa Kiswahili na Richard Mabala
Tuzo ya Hadithi Fupi ya Jumuiya ya Madola iko wazi kupokea hadithi hadi tarehe 1 Novemba 2025. Tuzo inakubali hadithi katika lugha ya Kiswahili. Ututumie hadithi yako hapa.